MAAFISA FANYENI KAZI KWA BIDII, MJIIMARISHE KIUTENDAJI – MEJA JENERALI ( MSTAAFU) MADAWILI
Meja Jenerali (Mstaafu) Zawadi Madawili ametoa wito kwa Maafisa wanawake wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania kufanya kazi kwa bidii ili kujiimarisha kiutendaji katika nafasi zao mbalimbali wanazohudumu.
Meja Jenerali Mstaafu Madawili ameyasema hayo tarehe 02 Mei 2025 katika kikao cha Umoja wa Maafisa wa kike wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wanaofanyia kazi Jeshi la Kujenga (JKT) pamoja na Kamandi nyingine ambacho kimefanyika katika Hoteli ya Ndege Beach Mbweni JKT Jijini Dar es salaam.
Aidha ameeleza siri ya kudumu muda mrefu katika Utumishi ni kufuata Misingi iliyowekwa ambayo ni pamoja na Nidhamu katika kazi, roho ya kupendana, Ushirikiano na Moyo wa kujituma kwa Maslahi ya Jeshi na Taifa kwa Ujumla.
Naye Mkuu wa Tawi la Logistiki na Uhandisi Jeshini ambaye ni Mlezi na mmoja wa Waasisi wa Umoja huo Meja Jenerali Hawa Kodi amesema Lengo la kuanzisha Kundi lilikuwa ni Kuweka Umoja na Mshikamano kwa Maafisa wanawake katika kusaidiana kwenye nyakati mbalimbali wakati na baada ya Utumishi.





Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Umoja huo Meja Ester Ryoba Amesema dhumuni la kikao ni kuwakumbusha Maafisa wanawake Majukumu yao Kijeshi pamoja na Kijamii kuendana na Nafasi walizonazo sambamba na kuwahimiza Kuhusu Shughuli za JKT zikiwemo kulea vijana na Uzalishaji Mali.
Maafisa hao wanawake sambamba na kushiriki kikao hicho pia wametembelea Vivutio vya Utaalii vilivyopo Mbweni JKT ambavyo ni Mbweni JKT Zoo, Mandhari ya Ndege Beach Hotel pamoja na kutembela Maeneo ya Fukwe ya Bahari ya Hindi inayopakana na kikosi hicho cha Jeshi.
Viongozi wengine walioudhuria Kikao hicho ni pamoja na Meja Jenerali Grace Mwakipunda (Mstaafu), Meja Jenerali Lilian Kingazi (Mstaafu), Brigedia Jenerali Sara Rwambali ( Mstaafu), Brigedia Jenerali Janeth Izengo, Brigedia Jenerali Solotina Nshushi, Maafisa Wakuu na Maafisa Wadogo
Umoja huo wa Maafisa wanawake Unajumuisha Maafisa wanaofanyia kazi JKT na ambao waliwahi kuhudumu JKT kwa sasa wamehamia katika Kamandi nyingine za Jeshi Ulinzi la wananchi wa Tanzania.