SUMAJKT yatembelewa na Ugeni kutoka Comoros
Ugeni kutoka Kisiwa cha Comoro, tarehe 06 Septemba 23 umetembelea Shirika la uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) lililopo Mlalakua jijini Dar es salaam.
Ujumbe huo wa watu watano ukiongozwa na Mhe. Gavana Sitti Farouata Mhoudine umefika Makao Makuu ya SUMAJKT kwa ziara ya kikazi na umepokelewa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Afisa Mtendaji Mkuu SUMAJKT Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Mhe. Gavana Sitti Farouata katika ziara hiyo amepata fursa ya kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUMAJKT kupitia Taarifa fupi iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa SUMAJKT.
Luteni Kanali George Wang’ombe.Taarifa hiyo imeonesha shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda na biashara sambamba na maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zikiwemo samani, matrekta, maji ya kunywa, huduma za ulinzi, huduma za usafi, maonesho ya mazao ya shamba yaliyofanyika Makao Makuu ya Shirika Mlalakua jijini Dar es sa- laam.
Mhe. Gavana Sitti Farouata amevutiwa na shirika kwa namna linavyotekeleza majukumu yake na amesema anapenda kufanya mkataba wa biashara na SUMAJKT katika biashara ya mchele na nyama vilevile katika ujenzi wa barabara.
“Napenda kuingia mkataba wa kufanya biashara na SUMAJKT, sasa mtaona kama wafanyabiashara wa Comoro muwaalike waje huku au nyie mje Comoro lakini nchini Comoro. Hakika mmefikia hatua ya kujua mbinu za kilimo nasisi mtufundishe jinsi ya kupata mazao mazuri.” alisema Mhe. Gavana.
Kwa upande wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa na Afisa Mtendaji Mkuu wa SUMAJKT Meja Jenerali Rajabu Mabele, ameushukuru ugeni huo kwa kufika SUMAJKT na kuonesha nia ya kufanya biashara na shirika hilo.
Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema SUMAJKT ipo tayari kwenda Ngazija kuonana na wafanyabiashara ili kufanya mashirikiano.
“tunashkuru sana kwa ujio wako na ugeni ulioambatana nao Mhe. Gavana, kama ulivyoona shughuli zetu sisi tuna furaha kuona umezifurahia bidhaa zetu, tupo tayari kushirikiana katika biashara na kutoa elimu kuhusu kilimo.Kihistoria sisi ni ndugu na tunashea utamaduni kwa hiyo hatu tashindwana na Tanzania ni yako na Ngazidja ni ya Watanzania”. Alisema.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata katika ziara hiyo alitoa historia fupi ya SUMAJKT na malengo yake huku akielezea sekta mbalimbali za shirika hilo Pamoja na makampuni na miradi.
“SUMAJKT ilianzishwa mwaka 1981 ikiwa na malengo mawili ya kuchangia gharama za shughuli za JKT na lengo la pili ni kujenga uchumi wa Tanzania.
Aidha Kanali Petro Ngata amesema shirika linatekeleza majukumu yake katika sekta nne zinazoendesha shughuli za biashara kupitia sekta hizo.
Kanali Ngata ametaja sekta hizo kuwa ni sekta ya ujenzi, sekta ya kilimo mifugo na uvuvi, sekta ya viwanda na sekta ya huduma na biashara zikiwa na makampuni kumi na tisa na miradi mitano.
Hiyo ni siku ya kwanza ya ziara ya Mhe. Gavana Sitti Farouata katika Makao Makuu ya SUMAJKT Mlalakua jijini Dar es salaam ambapo kesho anatarajiwa kuendelea na ziara yake katika kiwanda cha maji ya kunywa SUMAJKT Bottling Co. Ltd na katika kiwanda cha kushona nguo SUMAJKT Garments Co. Ltd vilivyopo Mgulani JKT jijini Dar es salaam.