GAVANA WA COMORO AVUTIWA NA BIDHAA ZA SUMAJKT
Gavana wa Kisiwa cha Ngazidja nchini Comoro Mhe. Mze Mohamed Ibrahim, ameridhishwa na Huduma na Bidhaa zinazozalishwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).
Mhe. Mze Ibrahim amebainisha hayo baada ya ziara yake Makao Makuu ya SUMAJKT Mlalakuwa Dar es salaam ambayo imelenga kuendeleza Uhusiano wa kibiashara baina ya SUMAJKT na nchi ya Comoro.
Katika ziara hiyo Gavana ameambatana na Wakurugenzi wa Chemba ya Biashara kutoka nchini humo, Pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Comoro nchini Tanzania.
Baada ya kuwasili Makao Makuu ya SUMAJKT Mhe.Mze Mohammed amepatiwa taarifa kuhusu SUMAJKT ambayo imeainisha maeneo ambayo wanaweza kushirikiana kibiashara ikiwemo Kilimo, Mifugo, Ujenzi, Usafirishaji, Maghala na uhifadhi wa bidhaa.
Ugeni huo ulipata fursa ya kuona baadhi ya Huduma na Bidhaa za Shirika hilo kupitia Maonesho Maalumu yaliyoandaliwa Kwa ajili yao katika Viwanja vya Makao Makuu ya Shirika hilo.
Aidha, Ugeni huo pia umetembelea Kiwanda cha Kutengeneza Taa za LED (SUMAJKT Skyzone Co. Ltd), ambacho kinatengeneza Taa za kutumia katika Viwanja vya ndege, mpira, Barabarani, mtaani, na kwenye majengo.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Brigedia Jenerali Petro Ngata kwa mapokezi mazuri, yote aliyotueleza pindi alipokuja Comoro tumeyaona na tumefurahi sana, tumeona SUMAJKT wanafanya Mambo mengi hivyo tutakaa na Wakurugenzi wa Chemba ya Biashara ili kuona ni maeneo gani tuanze kufanya kazi pamoja” amesema Mhe.Mze Mohamed Ibrahim.
Vilevile, Gavana amemshukuru Mkurugenzi wa SUMAJKT kwa kuwapa majibu ya ufumbuzi wa changamoto walizomueleza pindi alipotembelea nchini Comoro.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Brigedia Jenerali Petro Ngata, amemshukuru Gavana wa Kisiwa cha Ngazidja Mhe. Mze Mohamed, kwa kutembelea SUMAJKT na kufafanua kuwa ziara hiyo imetokana na ziara yake aliyofanya nchini Comoro hivi karibuni.
Brigedia Jenerali Ngata amebainisha kuwa ugeni huo umeridhishwa na shughuli zinazofanywa na SUMAJKT pia wameonesha nia ya dhati ya kushirikiana katika Biashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT ameuhakikishia Ugeni huo kuwa Shirika lipo tayari kushirikiana kibiashara katika maeneo ambayo watayaona yanafaa Kwa maslahi ya nchi zote mbili Tanzania na Comoro.