|

BRIGEDIA JENERALI NGATA AFANYA MAZUNGUMZO NA WAFANYABIASHARA NCHINI COMORO

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi ka Kujenga Taifa (SUMAJKT) Brigedia Jenerali Petro Ngata amefanya mazungumzo na Jumuiya ya wafanyabiashara kisiwani Comoro katika ukumbi wa Chambre de Commerce Ngazidja uliopo kisiwani humo.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 5 Septemba 2024, na wafanyabiashara wanaochukua bidhaa Tanzania na kuzipeleka nchini Comoro, Brigedia Jenerali Ngata alipata fursa ya kueleza shughuli mbalimbali zinazofanywa na SUMAJKT hususani katika Sekta ya Ujenzi, Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Aidha, Brigedia Jenerali Ngata ameeleza nia thabiti ya SUMAJKT kuhitaji kufanya kazi na wafanyabiashara hao katika nyanja ya Ujenzi na Kilimo.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Brigedia Jenerali Petro Ngata akikabidhi maji ya Uhuru Peak, ikiwa ni moja ya bidhaa zinazozalishwa na shirika hilo.

Kwa upande wa wafanyabiashara kisiwani Comoro wamesema kuwa wanapenda kufanya biashara na SUMAJKT ila changamoto inayowakabili wanaponunua mifugo kutoka Tanzania inafika kisiwani Comoro ikiwa imekufa na pia wanatozwa gharama kubwa kwenye mifugo.

Akijibu kuhusu changamoto hizo, Brigedia Jenerali Ngata amefafanua kuwa SUMAJKT itaona namna ya kufanyia kazi changamoto hizo zitakazokuwa ndani ya uwezo wa shirika ili kufanya biashara itakayonufaisha pande zote mbili.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania kisiwani Comoro, Mheshimiwa Said Yakub.

Baada ya kikao hicho ilifanyika hafla fupi iliyoandaliwa na Gavana wa Ngazidja Mhe. Mze Ibrahimu Hamad.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT akifanya mazungumzo na wafanyabiashara alipokuwa ziarani visiwani Comoro.

SUMAJKT imekuwa ikipanua wigo wa biashara kwa kufanya mashirikiano na wadau mbalimbali kwa lengo la kuzalisha faida zaidi ili kutekeleza majukumu ya uzalishaji wake.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia ziara ya Ujymbe kutoka SUMAJKT nchini Comoro ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Brigedia Jenerali Petro Ngata ambayo imelenga kuangalia fursa za biashara.

Similar Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *