SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA KUJENGA TAIFA
(SUMAJKT)

Viwanda

Kutokana na sera ya Serikali kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, Shirika liliitikia wito huo kwa vitendo kwa kuboresha viwanda vilivyopo na kuanzisha viwanda vipya. Kati ya mwaka 2016 hadi 2022 chini ya uongozi wa Maafisa Watendaji Wakuu (CEOs) kwa nyakati tofauti ambao ni Meja Jenerali Michael Isamuhyo, Meja Jenerali Martin Busungu, Meja Jenerali Charles Mbuge na Meja Jenerali Rajabu Mabele ambao wameweza kutekeleza sera hiyo kwa kuimarisha sekta ya viwanda.

Kabla ya kuanzishwa Shirika, shughuli za viwanda vidogovidogo zilikuwa zinafanyika ndani ya Vikosi vya JKT. Miongoni mwa Vikosi 21 Miaka 41 ya SUMAJKT FINALISED.indd 21 27/06/2022 11:32 AMMIAKA 41 YA SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA KUJENGA TAIFA (SUMAJKT) vya JKT vilivyokuwa vinajihusisha na viwanda ni pamoja na Mgulani ambapo kulikuwa na kiwanda cha ushonaji wa nguo, mahema, useremala, na utengenezaji wa sabuni,, Buhemba kulikuwa na kiwanda cha usokotaji na ufumaji wa vitambaa, Mbweni kulikuwa na kiwanda cha utengenezaji wa mitumbwi, na katika Kikosi cha Ruvu kulikuwa na kiwanda cha ushonaji wa nguo.
Baada ya kuanzishwa kwa Shirika mwaka 1981, miradi hii iliingizwa kwenye Shirika lakini haikufanya vizuri katika soko shindani kutokana na teknolojia duni na uhaba wa mitaji. Shirika katika jitihada za kukabiliana na changamoto za kiteknolojia na uhaba wa mitaji liliingia kwenye biashara ya ubia na makampuni ya nje kati ya Mwaka 2001 mpaka 2013. Makampuni hayo ni Pamoja na TANZASINO, CAMISUMA, CHINA TANZANIA GARMENTS na SUMAJKT ANIT ASFALT. Jitihada hizi za kuboresha sekta ya viwanda ndani ya JKT zilifanywa na Maafisa Watendaji Wakuu (CEOs) waliokuwepo kwa vipindi tofauti ambao ni Meja Jenerali Davis Mwamunyange, Meja Jenerali Abdulrahaman Shimbo, Meja Jenerali Martin Madata, Meja Jenerali Samwel Kitundu, Meja Jenerali Samwel Ndomba na Meja Jenerali Raphael Muhuga.

SUMAJKT ANIT ASFALT Co. Ltd

Hii ni kampuni ya ubia kati ya SUMAJKT na kampuni ya ANIT ASFALT kutoka nchini Uturuki. Shirika liliingia ubia na kampuni hiyo tarehe 07 Novemba 2015 kwa makubaliano ya kusaga na kuuza kokoto katika uwiano wa hisa 30% kwa SUMAJKT na 70% kwa ANIT ASFALT. Katika hisa hizo Shirika lilichangia kiasi cha fedha na kampuni ya ANIT ASFALT ilitoa mitambo. Kampuni hiyo inaendelea na uzalishaji wa kokoto katika eneo la Pongwe Msungura Mkoani Pwani.

Mbali na viwanda vya ubia, SUMAJKT ina jumla ya viwanda vitano (5) vinavyoendelea na uzalishaji ambavyo vipo katika maeneo mbalimbali nchini. Viwanda hivi ni:

1. SUMAJKT Chang’ombe Furniture Co. Ltd 
2. SUMAJKT Bottling Co. Ltd 
3. SUMAJKT Garment Co. Ltd 
4. Kiwanda cha Kuchakata Nafaka – Mlale, na
5. SUMAJKT Leather Products.

Aidha Viwanda viwili (2) vinakamilishwa tayari kuanza uzalishaji. Viwanda hivyo ni Kiwanda cha Taa za LED (SUMAJKT SKYZONE Co. Ltd) na Kiwanda cha Bati na Misumari (SUMAJKT Roofing Co. Ltd).

SUMAJKT Chang’ombe Furniture Co. Ltd

Kiwanda hiki kilinunuliwa na JKT tangu mwaka 1972 kama kiwanda kidogo cha kuzalisha samani kutoka kwa mmiliki binafsi aitwaye Luige na kukabidhiwa SUMAJKT mwaka 1982 kwa ajili ya mafunzo ya vijana na uzalishaji kibiashara. Baada ya maboresho, kiwanda hiki kilisajiliwa mnamo tarehe 12 Machi 2020 kuwa kampuni kwa jina la “SUMAJKT Chang’ombe Furniture Co. Ltd”. Kiwanda kinachomilikiwa na Shirika kwa asilimia mia moja. Lengo ni kutengeneza samani bora kwa ajili ya taasisi za Serikali, mashirika ya umma, makampuni na watu binafsi.

SUMAJKT Bottling Co. Ltd

Kiwanda hiki kinaozalisha maji ya kunywa yanayoitwa “Uhuru Peak Pure Drinking Water”, kilianzishwa rasmi tarehe 17 Aprili 2018 kwa jina la SUMAJKT Bottling Plant. Kilisajiliwa kuwa Kampuni kwa jina la SUMAJKT Bottling Co. Ltd mwaka 2020. Kiwanda kipo katika eneo la Mgulani JKT jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya kiwanda ni “The Peak of Natural Purity”.

Wazo la uanzishwaji kiwanda cha maji lilikuja baada ya SUMAJKT kutaka kufufua kiwanda kilichokuwa cha dawa za binadamu cha TANZANSINO kwa kushirikiana na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (TSSA). Tathimini ya kitaalamu ilifanywa kwa ushirikiano wa watendaji kutoka SUMAJKT, NHIF na MSD katika eneo la TANZANSINO na kushauri kuwa eneo halikidhi vigezo vya uanzishaji wa kiwanda cha kisasa cha dawa za binadamu. Kwa kuzingatia ushauri huo Shirika liliamua kuanzisha kiwanda cha maji ya kunywa katika eneo hilo.

Maji yanayozalishwa na kiwanda hiki ni sehemu muhimu ya huduma ya maji ya kunywa safi na salama inayotolewa kwa jamii vikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Serikali na watu binafsi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

SUMAJKT Garments Co. Ltd

Hii ni kampuni ya Shirika inayojishughulisha na ushonaji wa mavazi ya aina mbalimbali kwa ajili ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama, makampuni na watu binafsi kilichopo Mgulani JKT jijini Dar es Salaam. Kiwanda kilianza uzalishaji rasmi tarehe 22 Aprili 2017 na kusajiliwa kuwa Kampuni ya Ushonaji SUMAJKT Garments Co. Ltd mnamo 27 Februari 2020. Kiwanda kimenunua mashine mpya na kuendelea kutumia majengo na baadhi ya mashine zilizoachwa na Kiwanda cha CAMISUMA kilichofungwa mwaka 2010.

Kampuni imekua mstari wa mbele katika kupunguza gharama za upatikanaji wa mavazi ya kijeshi kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la kujenga Taifa(JKT), Jeshi la Akiba (JA) na Jeshi la Uhifadhi (TFS, TANAPA, TAWA na NCAA). Taasisi mbalimbali, mashirika na watu binafsi wanapata huduma ya ushonaji mavazi katika kiwanda cha SUMAJKT Garments Co. Ltd.

Kampuni ya maji ya SUMAJKT Bottling Co. Ltd na Kampuni ya Ushonaji ya SUMAJKT Garments Co. Ltd zilizinduliwa rasmi tarehe 17 Mei 2018 na Hayati Dkt. John Joseph pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Aidha, wakati wa uzinduzi huo ilitangazwa eneo la Mgulani JKT kuwa Kituo cha Uwekezaji cha JWTZ.

SUMAJKT Mlale Milling Co. Ltd

Hiki ni kiwanda cha Shirika kilichopo Mlale JKT Songea Mkoa wa Ruvuma. Kilianzishwa mwaka 2018 na kinajishughulisha na uchakataji wa nafaka za mahindi ili kuongeza thamani ya zao hilo kuleta manufaa ya kiuchumi kwa Shirika. Kiwanda hiki kinazalisha unga unaoitwa “Mlale Sembe” ambao unasambazwa sehemu mbalimbali nchini. Wazo la kuanzishwa kwa kiwanda cha Mlale lilitokana na hupatikanaji wa mahindi mkoa wa Ruvuma sambamba na mpango mkakati wa JKT kujitosheleza kwa chakula.

Kiwanda hiki kinazalisha unga bora wa mahindi kwa mahitaji ya Jeshi na jamii kwa ujumla.

SUMAJKT Leather Products

Kiwanda cha bidhaa za ngozi SUMAJKT Leather Products kipo eneo la Mlalakuwa, jijini Dar es Salaam na kinajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa za ngozi kwa ajili ya matumizi ya taasisi za ulinzi, shule, kampuni, pamoja na watu binafsi. Bidhaa zinazozalishwa ni pamoja na viatu, mikanda, mabegi na mikoba. Kiwanda hiki kilianzishwa rasmi tarehe 13 Julai 2017. Aidha, Kiwanda kilianza kwa kutumia moja ya majengo yaliyokuwa Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa Mlalakuwa Dar es Salaam na vyerehani vilivyokuwa vinatumiwa na Kampuni ya CAMISUMA kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za ngozi. Kwa sasa kiwanda kimefanikiwa kununua vyerehani na mashine za kisasa za kutengeneza bidhaa za aina mbalimbali.
Uzalishaji wa bidhaa za viwandani kwa sasa kwa ajili ya kufanya biashara ni mojawapo ya shughuli kuu ambazo zinaitambulisha Shirika katika tasnia ya Viwanda nchini. Shirika hili limekuwa kichocheo katika uzalishaji, uhamasishaji, na uchangiaji wa bidhaa katika sekta ya viwanda na hivyo kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa ajira kwa jamii ya Watanzania sambamba na kukuza uchumi wa viwanda.

Wizara ya Ulinzi

Jeshi la Wananchi la Tanzania

Jeshi la Kujenga Taifa

Shirika La Nyumbu

SUMAJKT© 2023

Imewezeshwa na Kutengenezwa na SUMAJKT

linkedin facebook pinterest youtube rss twitter instagram facebook-blank rss-blank linkedin-blank pinterest youtube twitter instagram