Ujenzi, Uhandisi na Ushauri
Sekta hii inatekeleza shughuli zake kupitia Kampuni ya Ujenzi (SUMAJKT Construction Co. Ltd), Kampuni ya Umeme (SUMAJKT Electric Co. Ltd) na Kampuni ya Ushauri Majenzi (SUMAJKT Consultancy Bureau Co. Ltd).
SUMAJKT Construction Co. Ltd (SCCL)
Hapo awali, kazi za ujenzi zilianza mwaka 1972 chini ya Brigedi ya Ujenzi (Builders Brigade) iliyokuwa na jukumu la ujenzi wa Makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa nchini. Pia ilishiriki katika Ujenzi wa nyumba za kupangisha za Shirika la Nyumba la Taifa (Slum Clearance Scheme) kati ya mwaka 1968 - 1973 kwenye maeneo ya Magomeni na Kinondoni jijini Dar es salaam.
Mwaka1992, “Builders Brigade” ilisajiliwa na Wizara ya Ujenzi na kubadili jina kuwa “National Service Construction Department (NSCD) ambayo ilisajiliwa kuwa Mkandarasi Daraja la Tatu. Mwaka 2004, baada ya kutekeleza kwa ufanisi mradi wa ujenzi wa nyumba 150 za watumishi wa Serikali huko Mbweni, Dar es Salaam, “National Service Construction Department” ilipandishwa daraja “Building Contractor” kutoka daraja la tatu kuwa daraja la kwanza.
Mwaka 2006 NSCD ilipata Usajili wa Ukandarasi wa Ujenzi wa Barabara Daraja la Nne (Civil Works Contractor Class Four) na Utandazaji Umeme Daraja la Nne (Electrical Contractor Class Four). NSCD imetekeleza kazi za ujenzi nyingi zikiwemo za kitaifa kwa weledi hivyo ilipandishwa madaraja na kupewa daraja la tatu katika “Civil Works Contractor” na daraja la kwanza katika “Electrical Contractor”.
NSCD ilipata usajili wa washauri wataalamu katika fani ya usanifu majengo (Architectural Firm) tarehe 22 Disemba 2017 na kusajiliwa katika kundi la
Wahandisi Washauri (Consulting Engineers) tarehe 19 Aprili 2018. Na mnamo, tarehe 24 Novemba 2018 NSCD ilisajiliwa na BRELA kuwa Kampuni kwa jina la SUMAJKT Construction Company Limited (SCCL).
Kampuni inatekeleza kazi za Ujenzi na Uhandisi kupitia kanda zake saba za Ujenzi ambazo ni Kanda ya Mashariki (Dar es salaam, Pwani na Morogoro), Kanda ya Magharibi (Kigoma, Katavi na Tabora) , Kanda ya Kati (Singida na Dodoma), Kanda ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma), Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro, Tanga, Manyara na Arusha), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa) na Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga na Geita).
Kwa pamoja kanda hizi za ujenzi zimefanikisha kutekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini. Miradi hii ni pamoja na Ujenzi wa nyumba za makazi, Majengo ya ofisi na biashara, Ujenzi wa barabara na madaraja, Ujenzi wa mabwawa ya maji na miundombinu ya maji, Kazi za umeme katika majengo na umeme mkubwa na Kazi za Uhandisi wa Mitambo. Pamoja na kutekeleza miradi ya kibiashara, Shirika hutekeleza pia miradi ya huduma kwa Serikali na jamii kama vile ujenzi wa ukuta unaouzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite, Mirerani mkoani Manyara, ujenzi wa majengo mbalimbali ndani ya Ikulu na ukuta unaozunguka Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, ujenzi wa jengo la Tume ya Uchaguzi. mkoani Dodoma, Hospitali ya Uhuru, Chamwino mkoani Dodoma na miradi mingine ya Serikali na jamii. Aidha Kampuni imekuwa ikitumia Teknolojia ya kisasa ya Ultimate Building Machine (UBM) katika ujenzi wa baadhi ya majengo ya Serikali na binafsi
SUMAJKT Consultancy Bureau Company Limited (SCBCL)
Kampuni ya Huduma za Ushauri Elekezi katika Majenzi (SCBCL) ni kampuni mpya iliyotokana na uwepo wa wataalamu katika Idara ya Ujenzi NSCD waliokuwa wakijihusisha na usanifu, ukadiriaji majenzi na usimamizi wa miradi ya ujenzi. Wazo la kuanzisha kampuni hii lilitokana na changamoto zilizokuwa zinajitokeza kwa vitengo vya Wasanifu (Architects), Wakadiriaji Majenzi (Quantity Surveyor) na Kampuni ya Uhandisi (Engineering Firms) kushindwa kuomba kazi za ushauri kupitia mwamvuli wa SUMAJKT CCL. Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Bodi za ERB na AQRB kampuni ya ukandarasi hairuhusiwi kufanya kazi za ushauri hivyo ikaonekana kuna haja ya kuanzisha kampuni inayojitegemea.
SCBCL ilipata usajili wa BRELA mnamo tarehe 21 Mei 2021 na kufanya mabadiliko ya majina ya vitengo mbalimbali ambavyo vimesajiliwa. Vitengo hivyo ni Wasanifu Majengo (Architects), Wakadiriaji Majengo (Quantity Surveyors) na Wahandisi Ushauri (Consulting Engineers). Kampuni inaendelea kufanya kazi na kampuni nyingine na asasi mbalimbali za Serikali na watu binafsi.
SUMAJKT Electric Co. Ltd (SECL)
Kampuni ya umeme SECL ilianza ikiwa ni kitengo cha umeme ndani ya NSCD mwaka 2004 na kusajiliwa katika daraja la nne la ukandarasi wa umeme. Mwaka 2020 kitengo hiki kilipanda hadhi na kusajiliwa katika daraja la kwanza na Contractors Registration Board (CRB) ili kutekeleza kazi zote za usambazaji umeme na mifumo ya umeme. Mwaka 2021, SECL ilisajiliwa na BRELA kuwa kampuni ya SUMAJKT Electric Co. Ltd.
Kwa ujumla, sekta ya ujenzi imekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini ikiwemo miradi ya kimkakati.