SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA KUJENGA TAIFA
(SUMAJKT)

Historia ya SUMAJKT

Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) lilianzishwa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.116 ya mwaka 1982 chini ya Sheria ya Uanzishwaji Mashirika ya Umma. Act No 23 of 1974 (Cap 119 RE 2002). SUMAJKT lilianzishwa kwa lengo la kufanya biashara na kuzalisha faida ili kuisaidia Serikali gharama za mafunzo ya Vijana wanaojiunga na JKT pamoja na Kujenga Uchumi wa Taifa.
SUMAJKT Katika Uzalishaji Mali limefanikiwa kuwa na shughuli ambazo zimegawanyika katika sekta zifuatazo: -
1. Sekta ya Ujenzi, Uhandisi na Ushauri.
2. Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
3. Sekta ya viwanda .
4. Sekta ya Huduma na Biashara.

1. Sekta ya Ujenzi, Uhandisi na Ushauri.

Sekta hii inatekeleza shughuli zake kupitia Kampuni ya ujenzi (SUMAJKT Construction Co. Ltd), Kampuni ya Umeme (SUMAJKT Electrical Co.Ltd) na Kampuni ya Ushauri majenzi (SUMAJKT Consultancy Bureau Co. Ltd).

a. Kampuni ya Ujenzi (SUMAJKT Construction Company Ltd).
Shirika kupitia kampuni yake ya Ujenzi ya SUMAJKT Construction Company Limited (SUMAJKT CCL) linatekeleza miradi ya Ujenzi kupitia Kanda zake saba (7) za ujenzi ​pamoja na miradi iliyopo chini ya Makao Makuu ya ​Kampuni ya Ujenzi, Kampuni linafanya shughuli zifuatazo: -

• Ujenzi wa Majengo
• Ujenzi wa Miundo mbinu ya barabara na Maji
• Ujenzi wa Miundo mbinu ya Umeme
• Inatoa huduma ya Ushauri wa Kihandisi na ​Usanifu Majengo.

SUMAJKT kupitia Kampuni yake ya Ujenzi imefanikiwa kutekeleza Miradi mbalimbali yenye maslahi Kitaifa katika ubora na kwa wakati, hali ambayo imeijengea Serikali na Taasisi binafsi kuzidi kuiamini.

b. Kampuni ya Ushauri majenzi (SUMAJKT Consultancy Bureau Co. Ltd).
Kampuni hii inatoa ushauri elekezi katika majenzi, usanifu wa majengo na barabara, kusimamia mikataba ya miradi ya ujenzi, kushauri namna bora na sahihi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi kwa kuzingatia gharama, ubora, muda na thamani ya fedha.

c. Kampuni ya Umeme (SUMAJKT Electrical Co.Ltd)
Kampuni ya Ujenzi wa Miundo mbinu ya Umeme (SUMAJKT Eletric Co.Ltd), ipo daraja la kwanza Kampuni hii inajishughulisha na kazi zote za umeme, “fire detection and alarm system” , Tehama(ICT), “service provider” za umeme, AC, Usambazaji wa umeme wa kati(33kv HT line na 0.4 kv LT Line), Ujenzi wa “substation”, “maintainance za transformer” na service zake.

d. Kunduchi stone Quarry
kampuni inajishughulisha na utengenezaji wa matofali, nguzo, “paving,” Fence Louvers”, “Cab Stones”.

2. Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi

a. Kilimo.
Shirika linajishughulisha na mashamba makubwa ya biashara ambayo ni shamba la Alizeti Hanang Mkoani Manyara, Shamba la mahindi na maharage Tanganyika mkoani Katavi, shamba la Mpunga Chita mkoani Morogoro, shamba la maharage Milundikwa mkoani Rukwa, Shamba USA River mkoani Arusha, na shamba la zaidi ya ekari 12,000 ambalo Serikali imelikabidhi kwa SUMAJKT awali lilikuwa likifahamika kwa jina la Kilombero Plantation Limited (KPL), katika shamba hilo utafanyika uzalishaji wa mpunga na mahindi, shamba hilo lina miundo mbinu ya kisasa ya umwagiliaji, mashine za kuhifadhi na kuongeza thamani mazao ya mpunga na mahindi.

b. Ufugaji
Shirika linajishughulisha na Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyama katika eneo la Oldonyo Sambu na katika kikosi cha Oljoro JKT mkoani Arusha, mafinga mkoani Iringa, na Misenyi mkoani Kagera.

c. Uvuvi
Shirika limeanzisha mradi wa SUMAPONICS katika kikosi cha Mbweni JKT Jijini Dar es Salaam ambao unahusika na utengenezaji na usambazaji mifumo ya kufuga samaki katika matenki (Recirculation Aquaculture System - RAS) sanjari na uzalishaji na usambazaji vifaranga wa samaki.

3. Sekta ya Viwanda

SUMAJKT kupitia Sekta ya Viwanda inaboresha viwanda vilivyopo na kuanzisha viwanda vipya. Shirika linamiliki Viwanda vifuatavyo:-

a. Kiwanda cha Ushonaji (SUMAJKT Garments CO.LTD).
Kiwanda kipo katika kituo cha uwekezaji cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mgulani JKT jijini Dar es salaam, Kiwanda hiki kinashona mavazi ya aina mbalimbali zikiwemo nguo za watu binafsi, sare za vyombo vya ulinzi na usalama, shule, kampuni na Taasisi mbalimbali.

b. Kiwanda cha Samani (SUMAJKT Chang’ombe Furniture Co.Ltd).
Kiwanda hiki kipo chang’ombe jijini Dar es salaam, kinatengeneza samani za kisasa zenye ubora kwa matumizi ya nyumbani na maofisini.

c. Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za Ngozi(SUMAJKT Leather Product)
kiwanda kinatengeneza Mikoba, Wallet, Viatu vya aina mbalimbali zikiwemo buti za vyombo vya ulinzi na usalama, viatu vya shule, viatu vya watoto na watu wazima, kiwanda kipo Mlalakuwa jijini Dar es salaam.

d. Kiwanda cha Maji ya Kunywa (SUMAJKT Bottling co.Ltd)
Kiwanda hiki nacho kipo Mgulani Dar es salaam ambacho kinatumia mitambo ya kisasa kuzalisha maji ya kunywa yajulikanayo kwa jina la Uhuru Peak na kinasambaza na kuuza maji yake katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

e. Kiwanda cha taa (SUMAJKT Skyzone Co.Ltd)
Hiki ni kiwanda cha ubia kati ya SUMAJKT na kampuni ya Everlight Africa Co.Ltd, Kiwanda kipo Makao Makuu ya SUMAJKT Mlalakuwa jijini Dar es salaam, kimekamilika kwa asilimia Tisini na Tano (95%) na mitambo yote imeishasimikwa, kikianza uzalishaji kitakuwa na taa za kisasa aina ya LED za barabarani, uwanja wa ndege, uwanja wa mpira, na bustani.

f. Kiwanda cha Mabati na Misumari (SUMAJKT Roofing Company Company Ltd).
Kiwanda hiki kipo jijini Dodoma, Mashine za Misumari ya kawaida na ya mabati pamoja na Mashine za kutengeneza mabati zote zimeishafika, Kiwanda kikianza uzalishaji kitakuwa kikizalisha Mabati ya aina ya Vigae, migongo midogo na mipana.

g. Kiwanda cha Nafaka Mlale (SUMAJKT Mlale Milling Co.Ltd).
Shirika lina kiwanda cha kuchakata mahindi Mlale JKT mkoani Ruvuma kinazalisha unga safi wa sembe unaojulikana kwa jina la SUMAJKT Mlale Sembe.

4. Sekta ya Huduma na Biashara.

a. SUMAJKT Port and Services Co.Ltd.
Kampuni hii inasimamia wafanyakazi wa kutwa katika Mamlaka ya Bandari (TPA) Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kigoma, kasanga na kemondo (Kagera), kyela (Mbeya) na Mwanza.

b. SUMAJKT Logistic Company Ltd.
Hii ni kampuni ya uondoaji na usafirishaji mizigo bandarini ambao msingi wa uanzishwaji wake ulikuwa ni kulipunguzia Shirika gharama za uondoshaji mizigo inayowasili bandarini. Kwa sasa linafanya kwa biashara ili kuongeza pato la Shirika.

c. SUMAJKT Catering Co.Ltd.
Shirika linatoa huduma za Kumbi ambazo ni Uhuru unaochukua watu 1000 na Umoja watu 500 kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo harusi, mikutano, semina na warsha, pia inatoa huduma ya chakula na vinywaji, kumbi hizo zipo eneo la mwenge jijini Dar es salaam.

d. SUMAJKT Auction Mart Co. Ltd
Kampuni hii inashughulika na Udalali, Ukusanyaji Madeni, Ushuru, Kodi na kukaza hukumu za mahakama.

e. SUMAJKT Guard Ltd.
Kampuni hii inatoa huduma ya ulinzi binafsi katika mashirika ya Umma, Taasisi na watu binafsi nchi nzima, mpaka sasa imeajiri idadi ya wafanyakazi 14704, vijana wazalendo waliopitia mafunzo ya awali ya JKT na Mgambo. Inahusisha
• Ulinzi wa milango (access control)
• Kamera za usalama (CCTV Camera)
• Mfumo wa ‘alarm’ katika vyombo vya moto
• Uzio wa umeme
• Mfumo wa ufuatiliaji magari
• Mfumo wa mafuta kwenye vyombo vya moto
• Mfumo wa alarm kwa ajili ya kudhibiti moto
• Mashine ya ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti moto
• Mashine ya ukaguzi kwa kutumia mionzi
• Ufungaji wa simu ya upepo (radio call)
• Walinzi wa usalama (security guard)
• Walinzi wa kutumia mbwa.
• Kufunga na kufungua mlango kwa umeme (automotive gates).


f. SUMAJKT Cleaning and Fumigation Co.Ltd.
Kampuni hii inatoa huduma ya usafi na umwagiliaji dawa za wadudu katika Taasisi binafsi, Mashirika ya Umma na kwa watu binafsi, ofisi zake zipo Mwenge jijini Dar es Salaam.

g. SUMAJKT Insurance broker Ltd.
Kampuni hii inatoa Bima ya Maisha na Bima zisizo za Maisha mfano bima ya afya, magari, nyumba, safari, kilimo, bima ya usafirishaji wa bidhaa, bima ya maisha, bima ya majeruhi,bima ya mashine, bima ya ujenzi na nyinginezo.

h. Shule ya sekondari Jitegemee na Kawawa
Shirika linatoa huduma ya elimu Kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kupitia Shule zake za Sekondari Jitegemee iliyopo Mgulani jijini Dar es salaam na Kawawa iliyopo Mafinga mkoani Iringa, jitihada zinaendelea kufanyika kuhakikisha ufaulu unaongezeka.

i. SUMAJKT Tower
Shirika lipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa Ujenzi wa jengo litakalo tumika kwa ajili ya biashara kwa kukodisha Taasisi mbalimbali na ofisi za SUMAJKT katika eneo la Medeli East Manispaa ya Dodoma. Jengo linajulikana kwa jina la SUMAJKT Tower.

j. Uuzaji na usambazaji wa zana za kilimo
Mradi huu umesaidia kukuza sekta ya kilimo Nchini kwa kuwauzia wakulima wadogo na wakubwa Matrekta na zana mbalimbali za kilimo. Kwasasa mradi unauza Matrekta aina ya New Holland na vipuli katika eneo la mwenge jijini Dar es salaam.

k. SUMAJKT Pharmaceuticals Co. Ltd
Shirika limeanzisha Kampuni ya SUMAJKT Pharmaceutical Co. Ltd (SPCL) kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali katika sekta ya Afya kama; huduma za Madawa, Vifaa tiba, Vifaa vya uchunguzi, vifaa vya Maabara na vifaa vya huduma za uchunguzi na Tafiti mbalimbali za Afya. Aidha inalenga kufungua viwanda vya madawa, na maduka makubwa ndani na nje ya Mkoa wa Dar Es Salaam ya kutoa na kusambaza huduma na vifaa mbalimbali vya Afya katika Vituo vya Afya na Maduka yanayouza Madawa na vifaa tiba. Kwasasa Ujenzi wa jengo la Kampuni hiyo unaendelea eneo la Mwenge jijini Dar Es Salaam.
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) linafanya jitihada kuhakikisha linazalisha bidhaa bora na kutoa huduma nzuri kwa wateja ili kuendana na soko la ushindani.

Wizara ya Ulinzi

Jeshi la Wananchi la Tanzania

Jeshi la Kujenga Taifa

Shirika La Nyumbu

SUMAJKT© 2023

Imewezeshwa na Kutengenezwa na SUMAJKT

linkedin facebook pinterest youtube rss twitter instagram facebook-blank rss-blank linkedin-blank pinterest youtube twitter instagram