SHIRIKA LA UZALISHAJI MALI LA JESHI LA KUJENGA TAIFA
(SUMAJKT)

Biashara

Sekta ya biashara na huduma inajumuisha miradi na kampuni tisa (9). Sekta hii inahusisha miradi na kampuni mbalimbali ifuatavyo:-

SUMAJKT Agri Machinery Project (Mradi wa Matrekta na Zana za Kilimo)

Mradi upo eneo la Mwenge Jijini Dar es Salaam. Mradi huu ni matokeo ya juhudi za Serikali zilizofanywa katika kutekeleza mpango wa kuinua sekta ya kilimo kupitia kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza” mwaka 2009 kutokana na juhudi za Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Shirika katika mpango huo lilipewa jukumu la kupokea kutoka Serikalini na kusambaza matrekta na zana za kilimo zilizonunuliwa kutoka nje. Hivyo, JKT kupitia Shirika lilianzisha mradi wa matrekta ili kutekeleza jukumu hilo la Serikali.

Mradi huu umekuwa msaada kwa wakulima tangu kuanzishwa kwake kwani wengi wamefaidika kupitia huduma ya Matrekta na zana zake. Aidha, huduma ya kusambaza matrekta, zana na vipuri vyake umesaidia kuanzisha mradi wezeshi wa kuuza matrekta, vipuri na zana za kilimo kwa njia ya fedha taslimu. Matrekta na zana hizo ni; Matrekta ya New Holland na FARMTRAC, majembe ya kulimia (Disc Plough), jembe la kuvunja udongo (Disc harrow), pump za umwagiliaji (Irrigation water pump) na tela (Trailer).

Mradi huu umewawezesha wakulima nchini kufaidika kwa kupata uelewa wa matumizi juu ya zana za kilimo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na ajira hasa maeneo ya vijijini. Pia, mradi unatekelezwa kwa kukusanya madeni kwa watu na taasisi zilizopewa Matrekta na vipuri.

SUMAJKT Guard Ltd

Hii ni kampuni tanzu ya Shirika ambayo inajishughulisha na utoaji huduma za ulinzi. Makao makuu ya kampuni ni Mlalakuwa jijini Dar es Salaam. Kampuni ilisajiliwa rasmi tarehe 20 Oktoba 2008 na kuanza kazi tarehe 01 Februari 2010 ikiwa na walinzi saba. Kampuni ilizinduliwa rasmi tarehe 28 Machi 2014, na kwa sasa kampuni ina walinzi zaidi ya 14,000 nchi nzima.

Malengo ya kuanzishwa kwa kampuni ni kutoa huduma ya ulinzi kwenye taasisi za Serikali, kampuni za umma na binafsi, kutoa ajira kwa vijana waliohitimu mafunzo ya JKT na mgambo. Pia, kampuni inatoa huduma za ulinzi kwa kutumia teknolojia za kisasa ambazo ni Ulinzi wa Milango (Access Control), Kamera za usalama (CCTV Camera), Mfumo wa ‘alarm’ katika vyombo vya moto, Mfumo wa ‘alarm’ kwa ajili ya kudhibiti moto, uzio wa umeme, Mfumo wa ufuatiliaji magari (Car Tracking System) na Mfumo wa mafuta kwenye vyombo vya moto. 

Nyingine ni Mashine ya ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti moto, Mashine ya ukaguzi kwa kutumia mionzi, Ufungaji wa simu ya upepo (Radio call), Kufunga na kufungua mlango kwa umeme (Automotive Gates), Ulinzi wa kutumia mbwa na huduma salama ya kusindikiza fedha. Sambamba na huduma hizo kampuni inatoa huduma ya magari ya kubeba wagonjwa na kuzima moto na uokoaji.

Katika kuboresha huduma za ulinzi SUMAJKT Guard Ltd inatoa huduma katika maeneo mbalimbali ya nchi kupitia kanda saba ambazo ni Kanda ya Mashariki, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini.

SUMAJKT Catering Co. Ltd

Hii ni Kampuni tanzu ya Shirika yenye Makao Makuu yake Mwenge, jijini Dar es Salaam. Kampuni inatoa huduma za kibiashara kwa kukodisha kumbi za sherehe, vyakula na mapambo katika matukio mbalimbali ya kiserikali na kijamii. Kampuni ilianza kama mradi mwezi Julai 2017 ikijulikana kwa jina la SUMAJKT Recreation & Catering Services kabla ya kusajiliwa rasmi mnamo tarehe 25 Machi, 2020.

Kampuni inaendelea kuboresha huduma zake ili kuweza kutoa huduma maeneo mengine nje ya Dar es Salaam.

SUMAJKT Port & Services Co. Ltd

Hii ni kampuni ya Shirika iliyosajiliwa rasmi mwaka 2020 kwa lengo la kusimamia shughuli za upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini na kuhakikisha usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini. mwaka 2017, ilianza kutoa huduma ya kuratibu na kusimamia wafanyakazi wa kutwa wanaoingia kufanya kazi ndani ya bandari ya Dar es Salaam. 

Mwaka 2019, mradi ulipewa kazi ya kutoa huduma hiyo katika bandari za Kigoma na Mwanza. Kwa sasa, imeingia makubaliano mapya ya kuratibu na kusimamia wafanyakazi katika bandari zote zilizopo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ambazo ni bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Tanga, Mtwara, Kigoma, Kyela, Kasanga, Bukoba na Kemondo.

Kampuni inaendelea kufanya kazi kwa weledi na uaminifu katika kutoa huduma na kujenga imani kwa watumiaji wa bandari zote nchini baada ya kuamini kuwa ni sehemu salama ya kupitishia mizigo yao.

SUMAJKT Cleaning and Fumigation Co. Ltd

Kampuni ya Usafi na Unyunyiziaji Dawa za Wadudu (SUMAJKT Cleaning and Fumigation Co. Ltd) yenye makao makuu yake Mwenge, jijini Dar es Salaam. Ilianzishwa kama kitengo cha usafi ndani ya SUMAJKT Guard Co. Ltd mwezi Septemba 2018 na kusajiliwa rasmi BRELA tarehe 14 Machi 2020. Kampuni inatoa huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi, mashirika, makampuni na watu binafsi.

Tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikijishughulisha na majukumu yake ya msingi ya kutoa huduma ya usafi na unyunyizaji dawa katika maeneo mbalimbali na inafanya juhudi kukuza huduma zake ili kufikia maeneo mengine ya nchi.

SUMAJKT Insurance Broker Co. Ltd

Kampuni hii ilianzishwa mwaka 2019 ili kutoa huduma ya bima za magari, afya, ajali, nyumba, safari za majini, biashara na maisha. Makao Makuu yake yapo Mgulani, jijini Dar es Salaam. Lengo la kuanzishwa kwake ni kusaidia Shirika katika kuongeza mapato kwa kutumia fursa ya wateja waliopo ndani na nje ya Jeshi. Kuanzishwa kwake kulitokana na hitaji la makampuni na miradi mbalimbali ndani ya Shirika ikiwemo miradi ya ujenzi, ulinzi pamoja na huduma ambazo husababisha Shirika kutoa fedha kwa makampuni mengine ya huduma za bima. 

Kutokana na hilo Shirika liliona fursa ya kuanzisha kampuni ya udalali na ushauri wa bima kwa ajili ya kusogeza karibu huduma hiyo kwa Shirika na jamii kwa ujumla. Kampuni inaendelea kujenga uwezo wa kufanya kazi za bima ndani ya Jeshi, miradi na kampuni zenye ubia na SUMAJKT. Kampuni inajikita kutanua soko kwa kutafuta kazi za nje ya Jeshi hasa kwenye taasisi, makampuni, na watu binafsi ambapo kazi zinatekelezwa kwa gharama iliyopangwa na Kamishna wa Usimamizi wa Bima Nchini kwa ufanisi mkubwa.

SUMAJKT Auction Mart Co. Ltd

Kampuni hii inajishughulisha na kazi za kukusanya ushuru (Levy Collection), ukusanyaji madeni (Debt Collection) na udalali wa minada (Auctioneers) baada ya kusajiliwa tarehe 11 Juni 2019. Makao Makuu yake yapo Mlalakuwa, jijini Dar es Salaam. Wateja wakubwa wa kampuni hii ni Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi mbalimbali za kifedha, mashirika madogo madogo ya kifedha na kampuni za biashara. 

Wazo la kuanzishwa SUMAJKT Auction Mart Co. Ltd lilitokana na Shirika kuwa na wateja ambao hawalipi madeni kwa wakati baada ya kupata huduma kutoka kampuni tanzu na hivyo kulazimika kuanzisha kampuni hii badala ya kuendelea kutumia kampuni binafsi kukusanya madeni. Mpaka sasa, kampuni imefanya kazi nyingi hasa kwenye ofisi za halmashauri za wilaya hapa nchini na mpango wa baadaye ni kuboresha huduma zake na kufikia maeneo mengine ya nchi.

SUMAJKT Logistics Co. Ltd

Kampuni hii ilisajiliwa mnamo mwezi Disemba 2021 kutoa huduma ya uwakala wa forodha na usafirishaji wa mizigo kwa JWTZ, JKT, SUMAJKT, mashirika ya umma na watu binafsi kwa lengo la kukuza huduma zake kibiashara. Makao Makuu yake yapo Mgulani, jijini Dar es Salaam. Kampuni ilianza kufanya kazi kama mradi mwaka 2013 ikijulikana kwa jina la SUMAJKT Clearing and Forwarding kwa lengo la kurahisisha uondoshaji na usafirishaji mizigo ya JWTZ na JKT (Inhouse Clearing and Forwarding).

Malengo ya baadaye ni kuboresha na kukuza shughuli zake kwa kupata vifaa wezeshi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

SUMAJKT Catering Co. Ltd

Hii ni Kampuni tanzu ya Shirika yenye Makao Makuu yake Mwenge, jijini Dar es Salaam. Kampuni inatoa huduma za kibiashara kwa kukodisha kumbi za sherehe, vyakula na mapambo katika matukio mbalimbali ya kiserikali na kijamii. Kampuni ilianza kama mradi mwezi Julai 2017 ikijulikana kwa jina la SUMAJKT Recreation & Catering Services kabla ya kusajiliwa rasmi mnamo tarehe 25 Machi, 2020.

Kampuni inaendelea kuboresha huduma zake ili kuweza kutoa huduma maeneo mengine nje ya Dar es Salaam.

Wizara ya Ulinzi

Jeshi la Wananchi la Tanzania

Jeshi la Kujenga Taifa

Shirika La Nyumbu

SUMAJKT© 2023

Imewezeshwa na Kutengenezwa na SUMAJKT

linkedin facebook pinterest youtube rss twitter instagram facebook-blank rss-blank linkedin-blank pinterest youtube twitter instagram