JENERALI MKUNDA AZINDUA MITAMBO YA MAJI SUMAJKT BOTTLING CO. LTD, AFURAHISHWA NA JITIHADA ZA SHIRIKA

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Jacob John Mkunda leo tarehe 16 Oktoba 2023 amezindua mitambo ya kuzalisha Maji ya kunywa ya Uhuru Peak katika kiwanda cha SUMAJKT Bottling Co. Limited kilichopo Mgulani JKT Jijini Dar es salaam.

Mitambo hiyo yenye thamani ya Tsh Bilioni Moja na milioni 800 inaanza kutumika rasmi kuanzia sasa ili kuongeza ufanisi wa kiwanda ikiwa ni Wingi wa Uzalishaji pamoja na kukidhi hitajio la huduma ya maji nchini.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi akikata utepe kuzindua maji ya Uhuru Peak katika chupa yenye muonekano mpya. aliyepo pembeni yake ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya SUMAJKT Bottling, Luteni Kanali Leah Mtuma

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Majeshi Jenerali John Mkunda ametoa shukurani kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa(SUMAJKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele kwa kumpa heshima ya kushiriki tukio hilo la kihistoria lenye lengo la Kukuza Uchumi nchini.

“Niwapongeze SUMAJKT kwa Ujumla kwa namna mnavyojitahidi kuboresha miundo mbinu ya makampuni, viwanda na miradi ili kuongeza Uzalishaji wenye tija na namna mnavyoshiriki majukumu mbalimbali ya kijamii hii ni ishara ya kuliletea Heshima Jeshi kwa Ujumla”

Aidha Jenerali Mkunda ameendelea kusema: “Serikali ya awamu ya sita kupitia Rais Samia ina matarajio Makubwa kwa Jeshi hasa JKT na SUMAJKT kwa namna mnavyotekeleza miradi mikubwa ya kitaifa kwa weledi na kwa wakati”

Kadhalika Jenerali Mkunda amesema kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na JKT Kupitia SUMAJKT kutekeleza MRADI wa ofisi ya Rais Ikulu ya Chamwino na Mji wa kiserikali mtumba jijini Dodoma na sasa limepewa jukumu lingine la Ujenzi wa Nyumba 5000 za makazi ya wananchi wanaopisha eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia katika Kijiji cha msomera Handeni Jijini Tanga, ni dhahiri kuwa wameaminiwa kupewa miradi mikubwa ya nchi.

Akizungumzia kuhusu huduma ya Uzalishaji itakayoanza kufanyika sasa Jenerali Mkunda amewasihi SUMAJKT kupitia kiwanda hicho kufanya Uzalishaji wenye faida ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama katika kuzalisha maji.

Sambamba na uzinduzi wa mitambo hiyo, Jenerali Mkunda pia Amezindua magari mapya yatakayotumika katika usambazaji wa maji kwa wateja, ambapo magari hayo ambapo magari hayo yamenunuliwa na SUMAJKT.

Naye Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali Hassan Mabena Kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa na Afisa mtendaji Mkuu wa SUMAJKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amemshukuru Jenerali Mkunda kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa mitambo ya kiwanda ambacho kina takribani miaka sita tangu kuanzishwa kwake.

“kiwanda kilianzishwa mwaka 2018 kikiwa na uhafifu wa Uzalishaji hali iliyopelekea shirika kuona umuhimu wa kufanya maboresho ili kuongeza Uzalishaji na mapato kwa shirika”

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT Kanali Petro Ngata amesema tukio hilo ni adhma ya kutimiza malengo ya shirika ya kuboresha, viwanda vingine, makampuni, na Miradi mbalimbali ili kukuza shirika kiuchumi.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Maafisa Jenerali, wakuu wa matawi , Wakurugenzi wa SUMAJKT na JKT kwa ujumla, Wakuu wa MIRADI, wakuu wa shule, Vyuo, Baadhi ya wakuu wa vikosi, wajumbe wa Bodi ya SUMAJKT, pamoja na watendaji wa SUMAJKT, na Waandishi wa habari.

Similar Posts